HRW: Askari usalama Msumbiji wanakiuka haki za binadamu.


Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limevituhumu vyombo vya usalama vya Msumbiji kuwa vinakiuka haki za binadamu katika operesheni zake za kupambana na ugaidi kaskazini mwa nchi.
Dewa Mavhinga, Mkurugenzi wa Human Rights Watch Kusini mwa Afrika amesema maafisa usalama wa Msumbiji wamewaua, kuwakamata na kuwatesa watu wanaoshukiwa kuwa wanachama wa genge la kigaidi linalofanya mashambulizi ya kikatili katika eneo la Cabo Delgado, lenye utajiri wa gesi na ambalo wakazi wake wengi ni Waislamu.
Amesema serikali inapaswa kukomesha mara moja ukatili huo na iwafikishe mbele ya vyombo vya sheria wahusika wa jinai hizo za kutisha dhidi ya binadamu.
Hivi karibuni serikali ya Msumbiji ilisema wapiganaji wa kundi la al Shabab wameua raia zaidi 50 wa nchi hiyo, mbali na kuchoma moto vijiji kadhaa na kuwalazimisha maelfu ya raia kukimbia makazi yao katika eneo hilo. Haijabainika iwapo kundi hilo la kigaidi la Msumbiji lina mfungamano wowote na kundi la kigaidi na kitakfiri al-Shabaab la Somalia au la.
Vijiji vya mkoa huo wa Cabo Delgado ulioko kaskazini mwa Msumbiji vimekuwa vikisumbuliwa na mashambulizi ya umwagaji damu ya wanachama wa kundi linalojiita Ahlu Sunna Wal Jamaa, ambao wakazi wa maeneo hayo wanawatambua kwa jina la al Shabab tangu mwezi Oktoba mwaka uliopita wa 2017.
Baada ya kushadidi hujuma hizo, serikali ya Msumbiji ilituma askari na polisi katika maeneo ya mpaka wa nchi hiyo na Tanzania na tayari imewakamata mamia ya washukiwa.

Leave a Comment