Bunge la Sudan launga mkono marekebisho ya sheria za uchaguzi, al Bashir kugombea tena.


Kiongozi wa muda mrefu wa Sudan, Omar Hassan al Bashir anakaribia kupata idhini ya kugombea tena kiti cha rais wa nchi hiyo baada ya wawakilishi wa Bunge la nchi hiyo kuunga mkono pendekezo la kufanyika marekebisho ya sheria za uchaguzi.
Marekebisho hayo yatakayoondoa ukomo wa muda wa urais yatamuwezesha Omar al Bashiri kugombea kiti cha rais wa Sudan baada ya kumalizika muda wake wa sasa mwaka 2020.
Kwa mujibu wa katiba ya sasa ya Sudan, al Bashir ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1989 haruhusiwi kugombea tena kiti hicho baada ya kumalizika muhula wake wa vipindi viwili ulioainishwa mwaka 2005 baada ya marekebisho ya sheria za uchaguzi.
Spika wa Bunge la Sudan, Ibrahim Ahmed Omar amesema amepokea barua iliyosainiwa na idadi kubwa ya wabunge wanaounga mkono marekebisho ya katiba yatakayomruhusu al Bashir kugombea tena kiti hicho.
Mapema mwaka huu chama tawala nchini Sudan cha Kongresi ya Taifa kilitangaza kuwa, kimemteua al Bashir kugombea kiti cha rais katika uchaguzi wa mwaka 2020.
Vyama vikuu vya upinzani nchini Sudan vimepinga hatua hiyo. Vyama hivyo pia vilisusia chaguzi za Rais na Bunge zilizofanyika mwaka 2015.
Rais Omar Hassan anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kwa tuhuma za kuhusika na jinai za kivita katika jimbo la Darfur.

Leave a Comment