Mahakama ya Rwanda yawaachilia Diane Rwigara na mama yake ikisema hawana hatia.


Mahakama mjini Kigali Rwanda imetangaza kuwa, mwanasiasa Diane Rwigara na mamake Adeline Rwigara hawana hatia na kwamba mashtaka dhidi yao hayana msingi wowote.

Mahakama imesema kwamba imefanya uamizi huo kutokana na kwamba upande wa mashitaka haukutoa ushahidi wa kutosha.
Wawili hao walishitakiwa kwa makosa ya kuchochea vurugu na mgawanyiko miongoni mwa wananchi wa Rwanda pamoja na kughushi nyaraka. Mwendesha Mashtaka alikuwa ameomba mahakama kuwapa kifungo cha miaka 22 jela.
Walikanusha madai hayo wakisema yana utashi wa kisiasa. Marekani imeishinikiza Rwanda kuondoa mashitaka hayo, lakini Rwanda imejibu kwamba haishinikizwi na yeyote na kuomba vyombo vya sheria visiingiliwe.
Uamuzi huo ulikuwa wa mwisho kuhusu maombi ya upande wa mashitaka ya kuwapa kifungo cha miaka 22 jela katika kikao cha mwisho mwezi uliopita, huku upande wa mawakili wao wakipinga maombi hayo na kusisitiza wateja wao kuachiwa huru mara moja.

Leave a Comment