Kiongozi wa Ikhwanul Muslimin ya Misri ahukumiwa kifungo kingine cha maisha jela.


Katika mwendelezo wa utoaji hukumu za adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa kiongozi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin, mahakama ya Misri imemhukumu Muhammad Badie na washtakiwa wengine watano hukumu ya kifungo cha maisha jela katika kesi nyingine iliyokuwa ikiwakabili.
Mahakama ya Jinai ya mjini Cairo jana ilitoa hukumu ya kesi ya mwaka 2013 inayojulikana kama “Matukio ya Ofisi ya Miongozo” inayomhusisha Dakta Badie na wanachama wengine wa Ikhwanul Muslimin na kutoa adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa washtakiwa hao.
Kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka wa serikali ya Misri, Badie na wanachama wengine kadhaa wa Ikhwanul Muslimin walitoa msaada kwa kundi moja la watu waliokuwa wamejizatiti kwa silaha na mada za miripuko na kupanga shambulio na hujuma iliyotekelezwa na kundi hilo.
Huko nyuma pia mahakama ya Cairo ilimhukumu Muhammad Badie vifungo vya maisha jela katika kesi nyingine kadhaa; na inasemekana kuwa adhabu ya kifungo cha muda wa zaidi ya karne moja imeshatolewa dhidi ya kiongozi huyo wa Ikhwanul Muslimin.
Baada ya rais wa sasa wa Misri, Abdel Fattah el Sisi kushika hatamu za madaraka kupitia mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2013, kuwakandamiza wapinzani na hasa viongozi, wanachama na wafuasi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin imekuwa moja ya ajenda zinazofanyiwa kazi na utawala wake.

Leave a Comment