Burundi yaiagiza UN ifunge ofisi yake ya haki za binadamu Bujumbura.


Serikali ya Burundi imeliagiza Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa lifunge ofisi yake iliyoko katika mji mkuu wa nchi hiyo, Bujumbura katika kipindi cha miezi miwili ijayo.
Msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, Ravina Shamdasani hii leo amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa, ni kweli walipokea barua jana Jumatano ya kutakiwa kufunga ofisi zao na kuondoka Bujumbura, lakini amesisitiza kuwa uamuzi huo umewasikitisha mno na wangelipenda kuendelea kushirikiana na Burundi.
Hatua hii inajiri miezi michache baada ya aliyekuwa Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Zeid Ra’ad al-Hussein kuitaja Burundi kama moja ya machinjio ya kuogofya ya haki za binadamu duniani.
Burundi ilisimamisha ushirikiano wake na ofisi hiyo ya UN tokea Oktoba mwaka 2016.
Burundi imekuwa ikighadhabishwa na hata kukosoa ripoti za Umoja wa Mataifa ambazo kila mara zimekuwa zikiielezea kidole cha lawama serikali ya Bujumbura kwa ukandamizaji na machafuko yanayoshuhudiwa nchini humo, tangu Rais Pierre Nkurunziza agombee muhula mwingine wa urais kinyume cha sheria mwaka 2015.
Watu 1,200 wanaripotiwa kuuawa katika ghasia na machafuko hayo tokea wakati huo hadi sasa.

Leave a Comment