Jeshi la Kongo DR lakabiliana na waasi; lauwa 18 mashariki mwa nchi.


Mapigano kati ya jeshi na waasi watiifu kwa Jenerali muasi wa zamani huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 18. Hayo yameelezwa leo na duru za jeshi la Kongo.
Zimeongeza kuwa waasi 14 na wanajeshi wa serikali wanne wameuliwa katika eneo la Fizi, katika mkoa tajiri kwa madini wa Kivu Kusini ambao mara kwa mara umekuwa ukishuhudia machafuko ya kikabila.
Mauaj hayo yamejiri katika mapigano kati ya waasi na wanajeshi wa serikali huku Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikijiandaa kwa uchaguzi wa rais wa tarehe 23 mwezi huu ambao uliakhirishwa mara kadhaa. Kapteni Dieudonne Kaserek msemaji wa jeshi wa mkoa mapema leo alisema kuwa waasi 12 wameuawa akiwemo naibu kamanda aliyefahamika kwa jina la Alida na kwamba wanajeshi watatu walizama majini mtoni wakati wa mapigano hayo. Mapigano hayo yamejiri kati ya jeshi la Kongo DR na wanamgambo watiifu kwa jenerali muasi wa jeshi William Amuri Yakutumba ambaye anampinga rais wa nchi hiyo Joseph Kabila. Baadhi ya duru zinasema kuwa wanamgambo hao wana mfungamano na waasi wa National Liberation Front wenye makao yao makuu katika nchi jirani ya Burundi.

Leave a Comment