Kiu na njaa yaua wahajiri 15 ndani ya boti, pwani ya Libya.


Maiti 15 za wahajiri zimepatikana zikiwa ndani ya boti katika pwani ya Libya, katika bahari ya Mediterania.
Raia wa Misri ambaye ni katika manusura wa ajali hiyo amesema leo Jumanne kuwa: “Tulikuwa wahajiri 25 ndani ya boti hiyo. Tulianzia safari mjini Sabratah, magharibi mwa Libya. Tulikuwa baharini kwa siku 12 bila chakula wala maji. Wenzetu 15 wamekufa baada ya kushindwa kuvumilia makali ya njaa na kiu.”

Mashuhuda wanasema wahajiri 10 walionusurika kwenye tukio hilo wapo katika hali mbaya ya kiafya na wamepelekwa katika hospitali na kituo cha Msalaba Mwekundu katika mji wa Misrata.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, jeshi la majini la Libya lilitangaza habari ya kuokoa wahajiri haramu 113 katika fukwe za magharibi mwa nchi hiyo, siku mbili baada ya wahajiri wengine 15 kufa maji katika bahari ya Mediterania.
Kutokana na kukosekana usalama na utulivu wa kisiasa baada ya matukio ya mwaka 2011 na uvamizi wa kijeshi wa Marekani na NATO nchini humo, hivi sasa Libya imekuwa kituo kikuu cha kusafirishia wahajiri haramu kutoka nchi mbalimbali za Afrika na Mashariki ya Kati.
Magenge ya magendo ya binadamu yanatumia fursa hiyo kuingiza nchini Libya makumi ya maelfu ya wahajiri haramu kila mwaka, wenye azma ya kwenda Ulaya kutafuta maisha.

Leave a Comment