Vigogo Acacia kortini kwa utakatishaji fedha.


Aliyekuwa Makamu wa Rais wa makampuni ya madini ya Pangea, North Mara, Bulyanhulu na Exploration Du Nord Ltee, Deogratias Mwanyika na mwenzake Alex Lugendo, jana walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Walisomewa mashtaka 39 yakiwamo ya kula njama, kughushi, utakatishaji fedha, dola za Marekani bilioni 374.2.
Vigogo hao pia wanadaiwa kukwepa kodi na kusababisha Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) kupata hasara ya dola za Marekani bilioni 112.2.
Katika hati ya mashtaka, ya kughushi yapo manane, kukwepa kodi manane na kutakatisha fedha 17.
Katika kesi hiyo, upande wa serikali uliwakilishwa na mawakili, Faraja Nchimbi, Jackline Nyantori na Shadrack Kimaro, wakati upande wa utetezi ukiwakilishwa na mawakili Hudson Ndusyepo, Gasper Nyika, Frola Jacob na Alex Mushumbusi.
Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mfawidhi, Calvin Mhina,Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi alidai kati ya Aprili 11, 2008 na Juni 30, 2017, washtakiwa hao kwa pamoja walitenda makosa hayo katika maeneo tofauti ya Dar es Salaam, Kahama, Tarime, Biharamulo, Johannesburg Afrika ya Kusini, Toronto, Canada na Uingereza.
Wanadaiwa wakiwa na ufahamu walitoa msaada wa kula njama, kupanga mkakati na kutekeleza vitendo vya uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.
Chanzo: Mtanzania 18/10/2018

Leave a Comment