Kibano Cha Walimu Wakware Chaja.


Seri kali imewasilisha bungeni muswada wa sheria utakaosaidia kuwabana na kuwadhibiti walimu watovu wa nidhamu, wanaokiuka maadili ya ufundishaji na wanaofanya mapenzi na wanafunzi katika shule za serikali na binafsi.
Akiwasilisha Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaaluma ya Walimu Tanzania wa mwaka 2018, bungeni Dodoma jana, Waziri wa E limu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako (pichani) alisema muswada huo unalenga kuweka muundo wa kisheria wa Bodi ya Kitaaluma ya Walimu Tanzania.
“Bodi hiyo itakuwa na jukumu la kuinua kiwango cha utaalamu wa ualimu kwa lengo la kuhakikisha walimu wanakuwa na viwango stahiki kitaaluma na wanafanya kazi yao kwa kuzingatia maadili ya ualimu,” alisema Profesa Ndalichako.
Alisema, mlengwa wa bodi hiyo ni mwalimu aliyefuzu mafunzo ya ualimu katika Chuo cha Ualimu na Chuo Kikuu kinachotambulika na mamlaka, aliyesoma katika ngazi ya Astashahada, Stashahada na Shahada ambaye anafundisha shule za awali, msingi, sekondari, chuo cha ualimu, chuo au kituo rasmi cha watu wazima.
“Bodi hiyo itasaidia kuwatambua walimu wote nchini wa shule za serikali na binafsi na kuwaajiri na kuwepo kwa mfumo madhubuti wa kuwadhibiti walimu watakaokwenda kinyume na maadali ya utaalamu wa ualimu,” alisema.
Alisema Bodi hiyo itafanya kazi kwa kuzingatia pia Itifaki ya Soko la Pamoja la Afrika Mashariki, ambayo inaruhusu wananchi wa nchi wanachama kuwa huru kufanya kazi katika nchi yoyote ya jumuiya hiyo, lakini awe mwanachama mwenye sifa za kitaaluma ili kufanya kazi katika nchi nyingine.
Profesa Ndalichako alisema, bodi hiyo ni muhimu kama chombo mahususi cha kusimamia utaalamu wa walimu, kama zilivyo Bodi ya Usajili Wahandisi, Bodi ya Usajili Makandarasi, Baraza la Usajili wa Madaktari na Madaktari wa Meno, Baraza la Wafamasia, Baraza za Uuguzi na Ukunga na Baraza la Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu.
Akiwasilisha maoni, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Peter Serukamba alisema kamati yake inashauri kufutwa kwa sharti la mwalimu anayesajiliwa kwa mara ya kwanza lazima awe amefanya kazi kwa muda wa mwaka mmoja.
“Kamati inashauri kufuta sharti hilo kwa mtu anayesajiliwa kwa mara ya kwanza asiwekwe sharti la kuwa na mwaka mmoja wa kufanya kazi kama sharti la kusajiliwa,” alisema.
Alisema kwa kufanya hivyo, kutatoa fursa kwa walimu wote waliomaliza kozi za ualimu, waweze kutambulika na Bodi na nchi kufahamu kwa kiwango gani ina hazina ya watu wenye taaluma ya ualimu. Kamati pia ilishauri kwamba, mwalimu atasajiliwa mara moja tu, kinachopaswa kuhuishwa ni leseni ya ufundishaji na si usajili wake.
“Uhuishaji wa usajili, kamati ilishauri kwamba ufanyike uhuishaji wa leseni na si usajili kwa kuwa usajili utafanyika mara moja na uhuishaji wa leseni utakuwa unafanyika mara kadhaa,” alisema Serukamba.
Kamati hiyo pia ilishauri kwamba katika katazo la mwalimu kufundisha kabla hajasajiliwa na Bodi, pia sharti hilo limjumuishe na mwajiri wake ambaye ataajiri mwalimu ambaye hajapata usajili na kupata leseni.
Kamati ilishauri kwamba mwalimu atakayekutwa anafundisha au amefanya makosa ya kufundisha bila kusajiliwa na Bodi, atakuwa amefanya kosa sawa sawa na mwalimu anayefundisha bila kuwa na leseni na adhabu yake ni kifungo cha miaka mitano au faini si chini ya Sh milioni tatu.
Chanzo:Habari Leo 06/09/2018

Leave a Comment