Ajali Yaua 6 Wakiwemo Watalii.


Watu sita wakiwemo watalii wanne na Watanzania, dereva na mpishi wamekufa papo hapo baada ya gari la utalii walimokuwa wakisafiria kupata ajali ya kugongana uso kwa uso na lori.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amesema ajali hiyo imetokea katika eneo la Mti Mmoja katika mji wa Nanja wilayani Monduli mkoani Arusha.
Gambo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Arusha amesema gari lililopata ajali ni lililokuwa likitoka jijini Arusha na kugongana uso kwa uso na lori lenye namba za Kenya lililokuwa likitoka Monduli Mjini.
Amesema kati ya wageni waliokufa watatu ni wanawake na mmoja ni mwanaume na Watanzania hao wawili miili hiyo iko katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru.
Gambo amesema, katika ajali hiyo kuna majeruhi wawili na walipata matibabu ya awali katika hospitali ya wilaya ya Monduli kabla ya kuhamishiwa katika hospitali ya rufaa ya Seliani kuendelea kupata matibabu zaidi.
”Kwa sasa ni mapema kutaja majina na nchi wanazotoka, ila ninachoweza kusema waliokufa katika ajali hiyo ni wageni wanne na Watanzania,” alisema Gambo.
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru, Omary Chande amekiri kupokea maiti hao na kuwahifadhi kwenye mochari ya hospitali hiyo ya mkoa.
Chande amesema hospital iinasubiri taratibu zingine za ndugu za wageni hao ili miili hiyo iweze kusafirishwa nchi wanazotoka.
Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Ramadhani Ng’azi alisema ajali hiyo ilitokea majira ya saa nne asubuhi katika eneo hilo la Mti Mmoja.
Amewataja waliokufa kwenye ajali hiyo, raia wa Tanzania ni dereva wa gari lenye namba za usajili T 418 AXX Toyota Land Cruiser mali ya kampuni ya utalii ya Tabia, Michael Fanuel (32) mkazi wa Arusha na mpishi Raymond Mollel (37) naye mkazi wa Arusha.
Hakutaja majina ya watalii waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo.
Kamanda huyo amesema dereva wa lori linalodaiwa kusababisha ajali hiyo, anashikiliwa na polisi na ni majeruhi aliyelazwa katika Hospitali ya Seliani aliyefahamika kwa jina la Abdilah Muhammed mwenye umri kati ya miaka 26 na 30 raia wa Kenya.
Amesema dereva huyo alikuwa akiendesha lori lenye namba za usajili KAY 6315 Mercedes Benz lenye tela namba ZB 8385 mali ya kampuni ya General Trading Transport Kenya. Gari hilo lilikuwa likitoka kupeleka chakula Kigoma kwa ajili ya wakimbizi na lilikuwa linarejea Kenya.
Chanzo:HabariLeo 03/09/2019

Leave a Comment