Miili ya watu zaidi ya 40 yaripotiwa kuopolewa Mwanza, Tanzania.


Miili ya watu 44 imeopolewa kutoka Ziwa Victoria baada ya kivuko kilichokuwa kimebeba mamia ya abiria kuzama jijini Mwanza Kaskazini magharibi mwa Tanzania.
Mkuu wa wilaya ya Ukerewe,Kanali Lucas Magembe amesema waliokolewa wakiwa salama ni watu 37, watu 32 wako hospitalini kwa ajili ya matibabu.
Juhudi za uokoaji ziliendelea mpaka majira ya saa mbili usiku ambapo zoezi hilo lilisitishwa kutokana na hali ya giza ambayo ilikuwa kikwazo kutekeleza zoezi hilo.
”Sababu nyingine ni kuwa nguvu kubwa inahitajika na inahitaji ushiriki wa jamii na watu wengi walikuwa wameshachoka, hasa wale wenye mitumbwi ambao walikuwa wakifika pale kubeba miili” alieleza Kanali Magembe.
Taarifa za awali zinaeleza kwamba kivuko hicho kilikuwa kimebeba mamia ya abiria.
Mkuu wa mkoa wa Mara, Adam Malima ameeleza kwamba maafisa kadhaa kutoka eneo hilo wakiwemo polisi na jeshi la majini wanaelekea kujiunga katika jitihada za uokoaji.
”Hatuijui hali halisi tunakwenda kuikagua kwanza halafu baadaye tutatoa tamko rasmi.
Malima ameeleza kwamba maboti ya polisi na jeshi yatashirikiana katika zoezi hilo.
”Tunaomba mungu atupe subira kwa wakati huu, na tusishuhudie idadi kubwa ya vifo’.

Leave a Comment