Jenerali Mwamunyange Aula Zimbabwe.


Mkuu wa Majeshi ya Tanzania mstaafu, Jenerali Davis Mwamunyange ameteuliwa na Rais wa Zimbabwe kuwa mmoja wa wajumbe wanaounda Tume ya watu saba kuchunguza vurugu, zilizotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu nchini Zimbabwe.
Uchaguzi wa Zimbabwe ulifanyika Julai 30 mwaka huu, ambapo Rais Emerson Mnangagwa alishinda kwa kupata kura asilimia 50.8 ya kura zote zilizopigwa.
Jenerali Mwamunyange alichaguliwa na Rais wa Awamu wa Nne, Dk Jakaya Kikwete kuwa Mkuu wa Majeshi mwaka 2007 na alitumikia nafasi hiyo hadi mwaka 2017.
Katika taarifa yake, Rais Mnangagwa alisema tume hiyo itaongozwa na aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Kgalema Motlanthe na itakuwa na wajumbe sita, ambao Mwanunyange ni mmoja wao.
Wajumbe wengine wa tume hiyo ni Mwanasheria kutoka Uingereza, Rodney Dickson aliyeiwakilisha serikali ya Kenya katika kesi ya vurugu za baada ya uchaguzi wa 2007 kwenye Mahakama ya ICC.
Mwingine ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Emeka Anyaoku kutoka Nigeria. Wajumbe wengine kutoka ndani ya nchi hiyo ni Profesa Charity Manyeruke, Profesa Lovemore Madhuku kutoka Chuo Kikuu cha Zimbabwe na Vimbai Nyemba, ambaye ni rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria wa Zimbabwe.
Rais Mnangagwa alisema tume hiyo, inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake miezi mitatu tangu kuapishwa kwa rais huyo. Awali, Rais Mnangagwa alisema amesikitishwa na vifo hivyo na kukilaumu chama kikuu cha upinzani cha MDC kwa vurugu hizo.
Waangalizi wa uchaguzi walilaumu jeshi kwa kujihusisha na vurugu hizo.
Katika taarifa yake hiyo, aliitaka tume hiyo kufanya kazi yake kwa weledi na kutoacha maswali ili ukweli wote ubainike.

Leave a Comment