Ijumaa, Mei 20, 2016


CameroonLeo ni Ijumaa tarehe 13 Shaaban mwaka 1437 Hijria mwafaka na tarehe 20 Mei mwaka 2016 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Cameroon ilitangaza kupata uhuru wake chini ya mfumo wa jamhuri na siku kama hii hujulikana kama siku ya taifa nchini humo. Kwa miaka kadhaa Cameroon ilikoloniwa na Ufaransa na Uingereza na mwaka 1946 Miladia, Umoja wa Mataifa ukaziweka chini ya mamlaka yake ardhi zote za nchi hiyo. Hata hivyo katika mwaka 1959 Miladia, udhibiti huo uliondolewa na mwaka mmoja baadaye Cameroon ikatangaza uhuru wake kwa jina la Jamhuri ya Cameroon. Kufuatia kutangazwa kuwa huru nchi hiyo, katiba ya Cameroon ikapasishwa kupitia kura ya maoni na nchi hiyo ikakubaliwa kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa.***

Katika siku kama ya leo miaka 82 iliyopita, Yemen ilipata kipigo mwishoni mwa vita vilivyojiri kati yake na Saudi Arabia baada ya nchi mbili hizo kuhitilafiana juu ya suala la mpaka na kupelekea kusainiwa makubaliano ya Ta’if kati ya Imam Yahya wa Yemen na Mfalme Abdul-Aziz wa Saudi Arabia. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Yemen iliikabidhi Saudia maeneo ya Najran, Jizaan na Asir kwa muda wa miaka 40.***

Miaka 114 iliyopita katika siku kama ya leo, Jamhuri huru ilitangazwa huko Cuba na wanajeshi wote wa Marekani wakaondoka katika ardhi ya nchi hiyo. Cuba ambayo iligunduliwa na Christopher Columbus tangu mwaka 1492 Miladia, ilikuwa koloni la Uhispania hadi kufikia mwaka 1898 Miladia. Lakini Marekani iliingiza vikosi vyake nchini humo na kuchukua nafasi ya mkoloni Uhispania baada ya kutoa pigo na kuifukuza nchi hiyo huko Cuba, kwa kisingizio eti cha kuwaunga mkono wanamapambano wapigania uhuru wa Cuba.***

Na siku kama ya leo miaka 210 iliyopita, alizaliwa John Stuart Mill mwanafalsafa na mchumi wa Uingereza. Stuart Mill alilelewa na kufunzwa na baba yake elimu za mantiki na uchumi na baadaye kuanza kuandika magazeti. Mill pia alichaguliwa kuwa mwakilishi wa bunge la Uingereza kwa duru moja. Vitabu muhimu vya Mchumi wa Kiingereza John Stuart Mill ni vile alivyoviita “Principals of Political Economy ” na “Principals of Political Science”. Mill aliaga dunia mwaka 1873. ***

Leave a Comment